MAZINGIRA
Mazingira ni vitu vyote vinavyotunzunguka vyenye uhai na visivyo na uhai. Vitu vyenye uhai ni pamoja na mimea na wanyama, lakini visivyo na uhai ni pamoja na hewa, maji na ardhi. Mazingira huweza kuundwa na vitu mbalimbali; yanaweza kuwa ya asili (kama misitu, milima, maziwa, mabonde, mito, bahari n.k.) au ya kutengenezwa na binadamu (kama majengo, viwanda n.k.).
Kutunza mazingira
Utunzaji wa mazingira ni hali ya kulinda na kuhifadhi vitu vyote vinavyomzunguka binadamu katika maisha yake. Vitu hivyo ni kama vile misitu, ardhi, mito, mabonde, wanyama, milima, hewa na bahari. Shughuli za utunzaji wa mazingira nchini Tanzania hufanyika katika ngazi mbalimbali. Serikali yetu ilianzisha ofisi na taasisi za kusimamia utunzaji wa mazingira
Serikali ya Tanzania mwaka 1983 ilianzisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuishauri serikali katika masuala yote yahusuyo usimamizi wa mazingira. Hivyo, tunapaswa kutunza mazingira yetu ili kulinda maisha yetu na maisha ya viumbe wengine.
Umuhimu wa kutunza mazingira
Mazingira safi na salama ni muhimu kwa ustawi wa afya zetu. Pia, hupendeza na kuvutia. Mazingira machafu huficha wadudu na viumbe wengine hatarishi. Wadudu na viumbe hao ni kama vile viroboto, inzi, mbu, panya na nyoka. Viumbe hawa hupenda kujificha katika maeneo machafu. Mazingira safi na salama huepusha maambukizi ya magonjwa ya ngozi, kuhara, malaria, tauni, kipindupindu na magonjwa mengine yatokanayo na mazingira machafu. Pia, huepusha uharibifu wa mazao mashambani, vyakula na mali nyingine nyumbani. Aidha, mazingira yaliyotunzwa hupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, tunapaswa kutunza mazingira ili kuendeleza na kurejesha ubora wake. Pia tunapaswa kutunza mazingira ili kuepuka madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira kwa mwanadamu na viumbe wengine.